Search This Blog

Sunday, June 20, 2010

Idadi ya watu inakua kwa kasi

SHIJA FELICIAN RFA
Ongezeko la Idadi ya watu ni la kasi sana

Tatizo la ongezeko la watu kuzaa bila mpango katika wilaya ya Kahama. haliendani na upatikanaji wa huduma za msingi za binadamu mfano na afya elimu na hivyo kusababisha watu wengi wa wilaya hiyo kukosa huduma hizo na kukabiliwa na umasikini hasa kwa jamii iliyopo vijijini ambayo inaamini kuwa uzazi wa watoto wengi ni ufahari.

Kwa mujibu wa takwimu za watu na makazi wilaya ya Kahama inakadiliwa kuwa na watu karibu milioni moja ikiwa na wastani wa ongezeko la asilimia 3.3% na kufuatia ongezeko hilo ni pato la kila mtu kwa mwaka ni shilingi 250,000/= huku idadi ya Hospital, vituo vya afya, madawa na vifaa tiba na watumishi wa afya haziendani na ongezeko hilo sambamba na Shule pamoja na samani zake na walimu kuzidiwa na wingi wa watoto.

Hali hiyo imebainishwa na timu ya waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kutoka mikoa ya kanda ya ziwa na Magharibi, waliopo kwenye washa ya siku nne ya mpango wa uzazi inayoendeshwa na shirika la EngenderHealth na mradi wa ACQUIRE Tanzania kwa kushirikiana na watu wa Marekani, walipotembelea Hospitali ya wilaya hiyo kuona upatikanaji wa tiba kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo na baadhi ya vituo vya afya na zahanati wilayani humo walipokuwa wakifuatilia suala la uelewa wa jamii kuhusiana na uzazi wa mpango unaotekelezwa na wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Wakiongea na waandishi hao kwa nyakati tofauti, baadhi ya akina mama waliokuwa kwenye kliniki hizo wamesema kuwa, suala la mpango wa uzazi wengi wao hawana mamlaka nalo isipokuwa waume zao ndio wenye mamlaka ya kupanga watoto wangapi wazae licha ya kuwa wanazaa kwa matatizo na kushindwa kuwahudumia watoto waliowazaa.

Kufuatia hali hiyo serikali kupitia mashirika mbalimbali ikiwemo watu wa Marekani katika mpango wake wa uzazi wa mpango, imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha kuwa, jamii inapata elimu ya kutosha juu ya kupanga uzazi kwa hiari hali ambayo inapunguza mimba zisizokuwa za lazima.

Kwa mujibu wa muuguzi mkuu wa hospitali ya wilaya ya kahama Bi. Grace Kalimenze amesema kuwa wastani wa akina mama wanane hadi kumi wanafungiwa kizazi kila siku wengi wao wakiwa wamezaa watoto kuanzia wanne hadi kumi hali inayohatarisha maisha yao endapo wataendelea kuzaa.

Muuguzi huyo amesema kuwa tangu mpango huo uanze mwaka 2008 vifo vya akina mama wajawazito na kuharibika kwa mimba imepungua kutoka vifo 66 mwaka 2008 hadi 46 mwaka 2009.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo shirika la EngenderHealth pamoja na mradi wa ACQUIRE Tanzania wanatoa elimu ya uzazi wa mpango kwa jamii kupitia vyombo vya habari na wadau wengine ili watu wanafamilia wapange kuwa na familia wanayoweza kuihudumia kulingana na uwezo walionao kwa kufuata njia salama za kuzuia mamba zisikzokuwa za lazima na kuondokana na baadhi ya mila zinazosema kuwa kila mtoto anakuja na riziki yake.

Mganga mkuu wa wilaya ya Kahama Dkt. Leonard Subi katika maelezo yake amesema kuwa kasi ya ufungaji kizazi inasua sua ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2009 ambapo wanawake waliofunga kizazi walikuwa 294 huku wanaume waliojitokeza kufunga kizazi walikuwa ni watatu tu, hali inayoonesha kuwa bado kuna mahitaji ya kupeleka elimu zaidi kuhusu uzazi wa mpango.

Changamoto zilizopo kutokana na ukusefu wa elimu ya uzazi ni pamoja na vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua na katika kipindi cha miaka miwili iliyopita akina mama 117 walifariki dunia idadi ambayo ni kubwa mno, hivyo waandishi wa habari kupitia mafunzo waliyopata kuhusu mpango wa uzazi wanapaswa kutumia taaluma yao kufikisha ujumbe huo kwa wananchi kwani wanauwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe huo.

MWISHO

No comments: