Search This Blog

Na Theonestina Juma &Lilian Lugakingira



“UGONJWA huu umeishanitesa kwa kipindi cha miaka 38 hadi hivi sasa, sijui unatibiwa wapi, ingawa sina uwezo wa kifedha hata nikipata sehemu wanakotibiwa watu wenye matatizo kama yangu, najiona kana kwamba niko tofauti na wanawake wenzangu” ndivyo, Bi. Thereza Kabyemela (65) anavyoanza kuzungumza na waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake kujua kuliko.

Mama huyo mkazi wa kitongoji cha Kyerunga kijiji na kata Ihanda, ambaye ana watoto saba, anadai alipatwa na ugonjwa wa fistula katika uzao wake wa nne, mwaka 1972 baada ya kujifungulia nyumbani.

Kabyemela ambaye anaonekana kuishi maisha duni, anasema alitumia dawa za kienyeji kutoka kwa wakunga wa jadi zilizomfanya kutoona umuhimu wa kujifungulia hospitali.

Akielezea jinsi anavyokabiliana na tatizo hilo kwa kipindi hicho chote hadi hivi sasa, ana wakati anapata matatizo hayo mme wake wa ndoa hakuwepo kwani tayari alifariki akiwa mjamzito.

Anasema baada ya kupatwa na tatizo hilo, alikwenda hospitali ya Nyakahanga ambapo alilazwa kwa muda wa mwezi mmoja na siku 20 lakini hakuweza kupona hadi sasa.

Hata hivyo kutokana na kifo cha mme wake, alilazimika kurithiwa na shemeji yake aliyemkumbuka kwa jina moja la Pastory ambaye alizaa naye watoto watatu akiwa bado anasumbuliwa na ugonjwa wa fistula.

Mama huyo ambaye aliyeonekana kuona kama neema kutembelewa na mwandishi wa makala haya, muda wote alioneshaa furaha hadi kufikia hatua ya kutokwa na machozi, huenda kutokana na kuwa na matumaini ya kupata msaada wa kutibiwa ugonjwa huo ambao umemfanya kuonekana kuwa yuko tofauti na wanawake wengine.

"Siamini kama ningeweza kutembelewa na mgeni kama wewe, wa kunipa mwanga wa kuweza kupata matibabu ambayo kwa uzee wangu huu nilikwisha amini kuwa ugonjwa huu unaonifanya nionekane tofauti na wanawake wenzangu, hauna tiba” anasema Kabyemela huku akiwa ameshika tama.

Hata hivyo safari hiyo haikuishia hapo ambapo mwandishi wa makala haya pia alimtembelea, Catherine Apolinary (71) mkazi wa kijiji na kata Ihanda, ambaye anadai aliishi na ugonjwa wa fistula kwa miaka tisa, kabla ya kupewa taarifa juu ya waganga waliofika katika hospitali ya Nyakahanga kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali.

Anasema taarifa za ujio wa waganga hao, ambao hakumbuki walitoka wapi, alizopelekewa na mtoto wa ndugu yake anayefanya kazi katika hospitali hiyo, zilimwezesha kupata matibabu katika hospitali hiyo.

Mama huyo ambaye anasema mtoto aliyemsababishia kupatwa na ugonjwa huo ana miaka takriban 20, anadai kuwa alipatwa na ugonjwa huo kutokana na kujeruhiwa wakati akijifungua hospitalini.

Apolinary anadai kuwa baada ya kupatwa na ugonjwa huo, alitengwa na mmewe ambapo alihamia kwa mke mdogo na kuwa wakati akija kwake alikuwa akilala kitanda kingine.

Pamoja na mama huyo kudai amepona, taarifa kutoka kwa majirani zake zinadai kuwa hajapona bali ameona aibu kueleza tatizo lake.

Mkunga mstaafu, aliyejitambulisha kwa jina la Fides Selestine anasema, anaamini kabisa kuwa mama huyo hajapona labda hakutaka kuwa wazi kutokana na kuona aibu wa kukabiliwa na tatizo hilo, ambalo hakulipata kwa kupenda.

Hata hivyo diwani wa kata ya Ihanda, Josiah Katanga alipohojiwa kuhusu kuwepo kwa wanawake wenye ugonjwa wa fistula katika kata yake, alikana na kudai hakuna hata mmoja, hali inayoonyesha kuwa baadhi ya viongozi hawajui matatizo yanayowakabili wananchi wanaowaongoza.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kuwepo kwa tabia ya wakazi wa kijiji hicho hasa wanaume kuoa wake wengi, ambapo kila mwanaume hukadiriwa kuoa wake zaidi ya wawili hali inayosababisha wanaume hao kukimbilia kwa mke mwingine endapo limetokea tatizo kama la fistula kwa mmoja wa wake zake.

Mratibu msaidizi afya ya uzazi na mtoto wa wilaya ya Karagwe, Esheza Mwombeki anakiri kuwepo kwa wanawake wanaopata ugonjwa wa fistula wakati wa kujifungua, na kuwa kudai kuwa wanawake wenye tatizo hilo wanapatikana kutoka maeneo ya vijijini hasa kutokana na huduma duni za afya.

Mwombeki anasema kuwa baada ya kupatikana taratibu za kuwasafirisha kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando iliyoko mkoani Mwanza zinafanyika na zinapokamilika wanapewa taarifa wanatoka vijijini na kupumzishwa kituo cha afya Kayanga kabla ya kupelekwa katika matibabu kwa gharama za halmashauri.

Anasema kwa kipindi cha mwaka jana walipatikana wagonjwa watatu ambao walisafirishwa hadi hospitali ya rufaa ya Bugando iliyoko jijini Mwanza na kutibiwa.



Anasema kwa robo ya kwanza ya mwaka huu (Januari-Machi) wamepata wanawake wawili mmoja kutoka kijiji cha Chamchuzi na mwingine sehemu za Ndama ambao waligharamiwa nauli na matibabu na baadae kurejeshewa fedha zao na kitengo kinachoshughulikia wagonjwa wa fistula katika hospitali hiyo.



Mwombeki anasema kuwa wakati mwingine wanapata madaktari wanaozungukia hospitali mbalimbali kutoa huduma za matibabu ambao hufika katika hospitali ya Isingiro ambapo wagonjwa wote hupewa taarifa na baadae kusafirishwa hadi katika hospitali hiyo na kupewa matibabu bure.



Anasema kuwa halmashauri hiyo inaendelea kutoa elimu ya uzazi salama kwa akina mama wajawazito ili waweze kuhudhuria kliniki na kujifungulia hospitali ili kupunguza idadi ya wanawake wanaopatwa na ugonjwa wa fistula wakati wa kujifungua.



Anatoa ushauri kwa akina mama ambao tayari wamepatwa na ugonjwa huo kuacha kujificha vijijini kwa kuona aibu na badala yake wajitokeze ili waweze kupatiwa matibabu.



…………………. Anna Sawaki akizungumza na gazeti hili anasema kuwa ugonjwa wa fistula unawapata wanawake wanaopatwa na uzazi pingamizi na kuchelewa kupata huduma wakati kujifungua., kutokana na huduma kuwa mbali, kutopata elimu ya afya na mila na desturi.



Sawaki anataja sababu nyingine zinazoweza kuchangia mama kupatwa na ugonjwa wa fistula ni mimba za utotoni na kuzaa katika umri mkubwa.





Mwisho



Na Lilian Lugakingira&Theonestina Juma



WILAYA ya Karagwe ni miongoni mwa wilaya saba za mkoa wa Kagera ambayo imeonekana kukumbwa na tatizo la kutokuwepo na huduma bora kwa wajawazito hasa kwa upande wa usafiri.



Hali hiyo imedhihirika wazi baada ya utafiti uliofanywa na waandishi wa habari chini ya Shirika lisilo la kiserikali la UTU Mwanamke linalojishughulisha na afya ya uzazi (baba, mama na mtoto), ambao walitembelea kata mbalimbali katika wilaya hiyo.



Miongoni mwa kata zilizotembelewa ni Ihanda ambapo iligundulika kuwa akina mama wajawazito wanalazimika kukodi magari kwenda hospitali kujifungua kutokana na kutokuwepo kwa huduma ya usafiri wa akina mama wajawazito katika kata hiyo.



Aidha tatizo hilo limesababisha asilimia kubwa ya akina mama kujifungulia majumbani hasa wasio na uwezo wa kifedha wa kukodisha magari ya biashara mfano taksi (taxi).



Mmoja wa wanawake ambao wamejifungulia nyumbani, Angelina Nicolaus (40) mkazi wa kata na kijijini cha Ihanda wilaya ya Karagwe, ambaye ana watoto wanne anasema mtoto wa kwanza na wa mwisho alimzalia nyumbani na kwamba watoto wawili tu ndiyo amezalia hospitalini.



Anasema, aliamua kujifungulia nyumbani kwa sababu hakuwa na tatizo lolote la kiafya wakati akiwa na mjamzito.Na kudai kuwa kitu kilichokuwa kikimpa ujasiri ni dawa za kienyeji alizozipata kutoka kwa wakunga wa jadi, kwa gharama nafuu na kumwezesha kujifungua salama.



Naye Joyce Joram (32) pia mkazi kijiji hicho, anasema ana watoto watano, ambao wote amewazalia nyumbani kwa sababu hakuona umuhimu wa kwenda hospitali maana hakuwa na tatizo lolote kiafya.Na kwamba kutokana kwa kipindi cha nyuma hakukuwepo kwa elimu na sheria za lazima mama mjamzito azalie hospitali hazikuwepo.



Hata hivyo wanawake hao wanasema kuwa endapo wangepata matatizo wakati wa kujifungua, wangeweza kupoteza maisha kutokana na kutokwepo kwa uhakika wa usafiri katika eneo lao wa kuwawahisha hospitali ambayo iko takriban kilomita 12 kutoka katika kijiji chao na Hospitali Teule ya wilaya ya Nyakahanga.



Wanasema kutokana na kukabiliwa na tatizo la usafiri, wananchi wenye uwezo kifedha ambao wanamiliki simu za mkononi hulazimika kuwa na namba za simu za madereva taxi na pikipiki kwa lengo la kuwasaidia endapo itatokea dharura.



“Mfano mimi nina namba za simu za madereva taxi watano, nikiwa na shida nawapigia hata majirani zangu wanapokuwa na shida nawasaidia kuwasiliana na madereva hao” anasema Angelina Nicolaus.



Wanasema pamoja na umbali huo uliopo wa kufuata huduma ya afya, katika kijiji hicho cha Ihanda hakuna zahanati, kituo cha afya, hospitali hata duka la dawa hali inayozidi kuhatarisha usalama wa afya yao.



Diwani wa kata ya Ihanda, Josiah Katanga anakiri kata yake yenye vijiji vitatu vya Lukole, Chonyonyo na Ihanda, kukabiliwa na matatizo mbalimbali likiwemo la kutokuwa na kituo cha afya na usafiri kwa mama wajawazito.



Katanga anasema akina mama wajawazito wanaohitaji huduma yoyote ya afya ikiwemo kujifungua wanalazimika kuifuata Nyakahanga ambayo ni hospitali teule ya wilaya ambayo iko umbali wa wastani wa kilomita 14.7 kutoka katani hapo.



Anasema pamoja na umbali huo, kata yake haina huduma ya usafiri ambapo akina mama wanajawazito hulazimika kukodi magari binafsi au endapo unapatikana msaada wa gari la serikali kutoka katika kata jirani, mhusika anatakiwa kuchangia mafuta.



Kwa upande wa watu wasio na uwezo wa kuchangia mafuta au kukodisha magari binafsi, anasema kuwa jamii inayowazunguka inalazimika kutoa michango kwa ajili ya kuwasafirisha, hali ambayo inaweza kusababisha madhara zaidi kwa mama huyo ikiwemo kupoteza maisha.



Hatua zaidi zinazochukuliwa na serikali ya wilaya anasema zinatolewa semina kwa jamii hasa kwa akina mama wajawazito kuwahi hospitali mapema kabla ya tarehe yake ya kujifungua aliyoandikiwa katika kadi yake ya kliniki.



Aidha tatizo hilo la usafiri pia limeonekana kuikumba kata ya Kayanga, ambayo ni makao makuu ya wilaya ya Karagwe, ambapo akina mama wajawazito wanaopewa rufaa kutoka katika kituo cha afya Kayanga kwenda hospitali teule ya wilaya, hulazimika kukodi magari binafsi kutokana na kituo hicho kutokuwa na usafiri.



Kaimu Mganga Mkuu wa kituo cha afya Kayanga, Ntongani Jaspa anasema licha ya kituo hicho kukabiliwa na tatizo la usafiri, pia hakina vitendea kazi vya kutosha, hali inayosababisha asilimia kubwa ya akina mama wajawazito kupewa rufaa ya kwenda kujifungulia hospitali ya Nyakahanga.



Anasema tatizo hilo huwalazimu watumishi wa kituo hicho kutoa fedha zao mfukoni kuwasafirisha akina mama wajawazito wasio na uwezo wa kukodi magari binafsi, hali ambayo inawapa wakati mgumu kutokana na kiwango kidogo cha mishahara.



“Inatulazimu tutumie ubinadamu, huwezi kukaa kimya na kumwacha mgonjwa akihangaika peke yake, hata kama mishahara yetu ni midogo…, hatuna fungu kwa ajili ya usafiri, dawa nazo zinachelewa kutumwa kutoka bohari kuu ya dawa (MSD) haya yote ni changamoto kwetu” anasema Jaspa.



Kuhusu mama wajawazito kujifungulia hospitalini, anabainisha kuwa kuwa lipo tatizo la akina mama wajawazito kutojifungulia hospitali. Kwani mwaka 2009 wajawazito waliohudhuria kliniki katika kituo hicho ni 802 ambapo waliojifungulia kituoni ni 428 na waliojifungulia njiani ni 25.



“Wajawazito 349 haijulikani walijifungulia wapi, sina uhakika kama wote walijifungulia nyumbani maana hapa karibu pia kuna hospitali ya wilaya, huenda wengine walikwenda huko” anasema Jaspa



Anasema kuwa kwa robo ya kwanza ya mwaka huu (Januari hadi Machi) wajawazito waliopokelewa kituoni hapo ni 275 ambao ni zaidi ya malengo yao ya kupokea wajawazito 253, ambapo waliojifungulia hapo ni 145 sawa na asilimia 52 na kati yao walioko chini ya miaka 18 ni saba.



Anasema kituo hicho cha afya ambacho kina wakunga 12 kinacho uwezo wa kuwalaza wagonjwa kati 25 hadi 30 wakiwemo na akina mama wajawazito, ambao husuburi muda wao wa kujifungua.



Afisa afya wa wilaya Beatrice Laurent anakiri kuwepo kwa tatizo la huduma za afya katika wilaya hiyo hasa kwa akina mama wajawazito kutokana na jiografia ya wilaya.



“Unakuta katika kijiji kuna zahanati lakini umbali wa mwananchi kutoka nyumbani kwake hadi ilipo zahanati ni kama kilomita 15, kuna mapori, milima, hakuna usafiri, hali ambayo inamwia vigumu mama mjamzito kuwahi kupata huduma” anasema Laurent.



Anasema kutokana na hali hiyo ili kunusuru maisha ya mama mjamzito na mtoto wilaya imetenga vyumba maalumu kwa ajili ya mama mjamzito kufika mapema kabla ya tarehe yake ya kujifungua aliyoandikiwa katika kadi yake ya kliniki.



Kwa upande wa usafiri anasema, wilaya hiyo ina magari sita ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ambapo magari matatu yalipelekwa vijijini vilivyoko mbali na hospitali teule ya wilaya, mfano kata Murongo ambayo iko mpakani mwa Tanzania na Uganda kilomita 126 kutoka huko hadi makao makuu ya wilaya na nyingine tatu ziko katika vituo vya afya.



Anasena kuwa kila gari la kubebea wagonjwa lina simu ya upepo (radio call) ambazo hutumika linapokuwa limetokea tatizo katika kituo jirani ambapo hulazimika kwenda kumchukua mgonjwa kwa sharti la kuchangia mafuta.

Anasema, utaratbibu wa wagonjwa kuchangia mafuta ulijadiliwa na kupitishwa katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe na kudai kuwa uchangiaji huo hauwahusu akina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.



mwisho