Search This Blog

Wajawazito wasifirishwa kwa Mikokoteni

WAJAWAZITO WASAFIRISHWA KWA MIKOKOTENI YA NG’OMBE


Na Anthony Mayunga-Serengeti.

MFUKO wa maendeleo ya jamii (Tasaf)wilayani Serengeti unategemea kuwakomboa wanawake wajawazito wa kijiji cha Iseresere wilayani hapa wanaosafirishwa kilometa 17 kwa njia ya mikokoteni yang’ombe kwa ajili ya huduma za uzazi.

Hali hiyo ambayo inadaiwa kuchangia vifo vingi vya akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutokana na kutokuwepo kwa huduma kijijini hapo sanjari na barabara imedumu kwa miaka yote toka uhuru.

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi kijijini hapobaadhi ya wakazi walisema kuwa kutokana na umbali huo na ukosefu wa barabara wanawake wengi wanajifungulia nyumbani,njiani na wengine hufa wakati wa kujifungua kwa kukosa huduma

Bhoke Semberi alisema kuwa wanalazimika kusafirishwa kwa mikokoteni ya ng’ombe kutokana na kuwa eneo hilo ni kama kisiwa hasa wakati wa masika gari haziingii kwa kuwa hakuna barabara.

“Wanawake tunadhalilika sana maana unasafirishwa kwa mikokoteni ,tunajifungulia njiani hadharani ,watoto wanakufa ,kwa njia hii toka nchi imepata uhuru hatukutakiwa kuwa hivi,”alisema kwa uchungu.

Alibainisha kuwa hata wanaokwenda huko katika zahanati wanalazimika kutembea siku nzima na hivyo kazi zingine za maendeleo hazifanyiki,

Nilipuuliza kama huwa wanasindikizwa na waume zao huspitaini alijibu "wanaume hawako tayari kutusindikiza ni mateso makubwa sana. Ingawa akina mama tungepata faraja sana ikiwa waume zetu wangekuwa wanatusindikiza kama tunavyosikia katika vyombo vya habari na kama alivyonihadithia rafiki yangu anayetoka Bukombe ambapo wanaume wamehamasika kuwasaidia wanawake wajawazito baada ya kupata mafunzo toka Shirika la EngenderHealth ambalo lipo chini nchi ya Mradi wa ACQUIRE Tanzania ambalo linapata ufhadili toka kwa watu wa Marekani (USAID)"



.

Alifafanua kuwa hata masuala ya uzazi wa mpango kwao ni ndoto kwa kwa kuwa hawapati huduma hiyo,na kuwa huenda zahanati yao ikikamilika itawasaidia kupata elimu .

“Zahanati ikikamilika huenda kukatokea mabadiliko na hata waume zetu wakapata elimu ,pamoja na shida ya huduma za afya hapa kuzalina ni kila mwaka ,”alilalama.

Alisema kuwa wameamua kujitolea kuhakikisha zahanati hiyo kupitia Tasaf inakamilika ili iweze kuwakomboa kwa kuwa nje ya kuibua mradi huo ,halmashauri haijaonyesha juhudi zozote ikizingatiwa hata barabara hakuna.

Diwani wa kaya hiyo Rashidi Mugare (ccm)alikiri kuwepo kwa tatizo kubwa kijijini hapo na kuwa hata baada ya kuibua mradi wa zahanati na kukubaliwa jamii ilijitokeza kwa nguvu zote kuhakikisha wanajenga na kukamilika ili kupunguza ukubwa wa tatizo.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Mussa Ng’ombe alikiri kuwepo kwa vifo vingi na kuwa hata hivi karibuni mjamzito mmoja alinusurika kufa kwa kukosa huduma toka saa 4asubuhi hadi saa 11 jioni.

“Alifikishwa hospitali ya mkoa na kujifungua ,lakini aliugua Festula kwa ujumla hali si nzuri,tunapoteza watu wetu kwa kukosa huduma ,kwa miaka yote hapa tunaishi kama tuko kisiwani,tunategemea zahanati hii kutukomboa,”alisema.



Katibu wa kamati ya Tasaf Joseph Machumbe alisema kuwa mradi huo unajengwa kwa kasi kwa kushirikisha makundi yote kwa kuwa tatizo hilo linawakabili wote hapo kijijini.

“Ushiriki wa jamii ni mkubwa sana hasa wanawake kwa kuwa wanatambua wazi kuwa tatizo ni letu na hakuna wa kutusaidia maana vifo na matatizo mengine kwa watoto na wajawazito ni kiashiria wazi kuwa kama hakutakuwa na juhudi za makusudi basi tutakwisha,”alisema.

Mratibu wa Tasaf wilaya Juma Wambura Kobeche alisema kuwa mradi huo ulikubaliwa baada ya kukidhi vigezo na hali halisi,na kuwa jamii imeshiriki vema katika utekelezaji wa mradi kwa kuwa tatizo hilo linawagusa wananchi wote.

Alidai kuwa kwa hatua ya awali wamefanikiwa kutekeleza kama ilivyopangwa,nakuwa halmashauri imekubali kuwapa fedha mil.7 kukamilisha,ingawa hazitatosha lakini Tasaf makao makuu wamekubali kutoa fedha ili kukamilisha kila kitu na waweze kuanza.

Hata hivyo pamoja na serikali kupitia ilani ya uchaguzi ya Ccm ya mwaka 2005 ya kuhakikisha inaboresha huduma za afya,na kupunguza vifo kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka 5 bado hali ni tete.

Halikadharika kupitia mkukuta na nguzo zake tatu ikiwemo ya huduma za afya kupewa kipaumbele ili kuinua kiwango na ubora wa maisha ikiwemo upunguzaji wa vifo vya akina mama na watoto toka 578 hadi kufikia 450 bado haijafanikiwa.

Aidha hata malengo ya mellania (MDG) lengo la 5 la kuboresha huduma na kupunguza vifo kwa robo tatu kati ya 1990-2015 bado ni changamoto kuwa bila zahanati na wataalam bado tatizo litaongezeka badala ya kupungua.

mwisho