Search This Blog

Saturday, July 10, 2010

Mimba za utotoni
Picha: Mwalimu Pili Maximiliani, Mkuu wa Shule ya Kamnyang'anyo sekondari, Wanafunzi wa Shule ya Kamnyang'anyo, Dr Rashidi Shemsanga akiongea na waandishi habari


Uongozi wa Kijiji wazira kushughulikia mimba za utotoni

Na Charles Kayoka

Uongozi wa kijiji cha Magamba, kata ya Kwaluguru, wilayani Handeni wamesema wana mpango wa kutangaza kwa wanakijiji kuwa hawatapokea tena kesi za mimba za wanafunzi kutokana na kukosa ushirikiano na polisi na mahakama wilayani.
Afisa mtendaji wa Kijiji, Hemedi Mbelwa, mtendaji wa kijiji hicho, anasema wameamizia kuitisha kikao cha kamati ya kijiji ili kufikia uamuzi huo na kutoa tangazo kwa wanakijii kuwa kuanzia hapo wanakijiji wasiletea malalamiko tena juu ya watoto wao kupewa mimba.
“hili suala linatuletea ugombanishi na jamii. Tunawakamata wahalifu, lakini polisi na mahakama inawaachia wahalifu ambao wakirudi kijijini wanatuakashifu na tunaonekana sisi wote ni wapumbavu,” alisema.
Aidha mwalimu mmoja wa shule ya msingi aliwahi kukamata mwanamume mtu mzima akifanya mapenzi na msichana wa shule anakofundisha alisema kuwa hatataka tena kujihusisha na suala la mapenzi na mimba za wanafunzi kwa sababu “hakimu wa wilaya aliniuliza maswali ambayo yamenikatisha tamaa.”
Anasema yeye kwa kushirikiana na mgambo mmoja wa kijiji waliweza kumkamata mwanaume huyo na kumfikisha mbele ya sheria kwa matumiani kuwa hatua za kisheria zingechukuliwa, lakini badala yake alionekana kutotoa ushirikiano na hivyo “nikajiona ni mpumbavu kabisa. Kuanzia sasa sitaki tena kujihusisha na masuala haya.”
Hassani Mwachibuzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu hatua wanazozichukua kudhibiti mimba za utotoni, alisema kuwa wao hawana majibu kwani hayo yanayotokea ni matokea ya kushindwa kuwa na mikakati ya ziada.
“Huenda nyie mliekwenda huko vijijini na kuongea na wananchi mtupatie mapendekezo ya kutatua haya masuala. Maana sisi tumekuwepo hapa wakati wote na kama mnaona mambo siyo mazuri, basi mjue hapa ndio mwisho wa uwezo wetu,” alisema Mkurugenzi.
Akiongea na waandishi wa habari Kaimu Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Handeni, Dr. Rashid Shemsanga alikiri kuwa tatizo la mimba la utotoni lipo, “na nimewahi kushuhudia watoto wa miaka kumi na tatu wakijifungua hapa. “
Alisema kati ya mwezi Januari 2010 hadi Juni, kwa mujibu wa takwimu za hospitali, jumla ya watoto wa kike 141 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 18 walikuja hospitali ya wilaya kujifungua.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Kamnyang’anyo, Bi Pili Maximilian, alikiri kuwepo kwa tatizo la watoto kupata mimba na kuwa mwaka jana jumla ya wanafunzi wanane walipata mimba shuleni kwake.
Wanafunzi waliohojiwa walikiri kuwa wanafunzi wa kike na wa kiume wanafanya mapenzi wakiwa na umri mdogo wakisukumwa na tamaa ya vitu vizuri, umasikini na wazazi walio masikini na wenye watoto wengi kushindwa kutimiza mahitaji ya watoto wao. Na kuwa wasichana wanaoishi gheta katika sekondari za kata ndio wanaoathirika zaidi.
Mwisho.

No comments: