MJAMZITO ANYIMWA HUDUMA ,AJIFUNGULIA KICHAKANI ,MTOTO AFARIKI BAADA YA
MUDA MFUPI,
Na Anthony Mayunga-Serengeti.
MJAMZITO mmoja mkazi wa kijiji cha Maji moto kata ya Busawe wilayani hapa Esther Thadeus amelazimika kujifungulia kichakani baada ya kunyimwa huduma na muuguzi wa zahanati ya kijijini hapo na kupelekea mtoto kufariki muda mfupi baada ya kujifungua.
Tukio hilo ambalo limewastua watu wengi linadaiwa kutokea juni 28 mwaka huu majira ya saa 7 mchana na linadhihirisha kuwa vifo vingi vya wajawazito na watoto wadogo kutokana na utendaji mbovu wa wauguzi na wakunga.
Akisimulia mkasa huo ambao umelaaniwa na wakazi wa kijiji hicho Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Johanes Masirori alisema,tukio hilo lilifanywa siri kubwa na uongozi wa zahanati hiyo na hivyo
hakuweza kujua mapema.
"Nilipata taarifa julai saba nikafuatilia mama aliyepata matatizo na mashuhuda wakaniambia,muuguzi alipoulizwa alionekana kuwa na jeuri ile ile wala hajutii kitendo hicho,nilimtaarifu Mkurugenzi mtendaji juu ya tukio hilo,"alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa Mama huyo inadaiwa alifika zahanati hapo akiwa tayari katika hatua ya kujifungua ,lakini muuguzi huyo ambaye yukopekee yake alidai hana nafasi ya kumhudumia.
"Akina mama walimsihi amsaidie mwenzao ,lakini majibu yake yanadaiwa yalikuwa mabaya ,kwamba wasome nao waweze kumsaidia maana yeye ana kazi zake,"alibainisha.
Kutokana na majibu hayo mama huyo alizidiwa na kufikia hatua ya kuhisi haja kubwa ndipo akaenda kichakani ,kabla ya yote akajifungua huku akisaidiwa na wanawake wenzake.
"Hawakuwa na vifaa hivyo walihangaika sana ,maana kondo la nyuma liligoma kutoka,wengine wakalazimika kutafuta wembe madukani ,hata hivyo mara baada ya kutoka kwa mtoto aliaga dunia kutokana na kile kinachodaiwa kuzidiwa kwa kushindwa kutoka mapema,"alisema Mwenyekiti.
Hata hivyo licha ya tatizo hilo kujitokeza muuguzi huyo Devota Thobias hakuweza kumhudumia hali iliyopelekea waende nyumbani kisha kumpeleka kituo cha afya cha Iramba kwa ajili ya matibabu zaidi.
Akizungumzia utendaji wa muuguzi huyo Mwenyekiti alisema kuwa yupo hapo toka mwaka 1984 na ameolewa na aliyewahi kuwa diwani wa kata hiyo ,hivyo anafanya kazi kadri anavyojisikia wala si utaratibu.
"Malalamiko ni mengi juu ya utendaji wake ,anachukua muda mwingi kuuza duka lake la dawa ,wagonjwa mpaka wamfuate kwake hata muda wa kazi,anatuhumiwa kuuza kadi kwa wajawazito ,kuwatoza fedha hata watoto chini ya miaka mitano,tumelalamika hakuna utekelezaji,"alisema.
"Kuna madai hata ya upotevu wa dawa katika zahanati yetu katika mazingira tete,kumbe anahamisha na kuuza dukani kwake,wakuu wake wanaambiwa lakini hakuna hatua yoyote,"alisema.
Alisema Mkurugenzi julai 6 mara baada ya kupata taarifa aliunda tume iliyoundwa na Shadraka Isalo Mwenyekiti,Peter Shilingi katibu wa afya wilaya,Muuguzi mkuu Nyeura,na Winifrida Mwolo mkuu wa kitengo cha mama na mtoto ambao julai 7 walianza kazi yao.
Mkurugenzi mtendaji Kimulika Galikunga alipotafutwa kwa njia ya simu licha ya kuita hakuweza kupokea,na hata alipotumiwa maswali kwa njia ya ujumbe hakuweza kujibu.
Naye muuguzi huyo anayetuhumiwa na sakata hilo alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya mkononi hakuweza kupokea licha ya kuita kwa muda mrefu.
Baadhi ya wakazi wa Iseresere kata hiyo ambao wanatembea kilometa zaidi 17 kufika zahanati hapo ,tena wakitumia usafiri wa mikokoteni ya ng'ombe kupeleka wajawaito walidai kutokana na huduma mbaya hujifungulia majumbani .
Walisema kuwa vifo vya wajawazito na watoto wadogo ni vingi kwa kuwa wanalazimika kusafirisha wajawazito kwenda kituo cha afya Iramba ama hospitali ya mkoa Musoma badala ya kwenda hapo kutokana na huduma mbaya.
Juhudi za kumsaka mama aliyepata matatizo na muuguzi huyo zinaendelea ili kujua kwa undani mkasa huo unaokinzana na mikakati ya serikali ya kuhakikisha wanapunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
No comments:
Post a Comment