Search This Blog

Wednesday, July 14, 2010

Story za Handeni

Burhani Yakub,Handeni.

ALIYEWAHI kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni,Luteni Mstaafu Winfred
Ligubi,amekumbukwa na wanawake wa kwa kitendo chake alichofanya
kumpiga makofi mwanaume aliyemkuta akitembea kwa maringo huku mkewe
mjamzito akiwa amebeba mzigo wa kuni na mtoto mgongoni.

Pongezi hizo walizitoa juzi walipokuwa wakizungumza na waandishi wa
habari waliokuwa Wilayani hapa kujifunza juu ya unyanyasaji,unyanyapaa
na ukatili wa kijinsia na masuala ya ukimwi yanayoendeshwa na Chama
cha waandishi wa habari za ukimwi (Ajat)

Wanawake hao wa kata ya Chanika,Wilayani hapa wamesema kuwa alipokuwa
Mkuu wa Wilaya moja Mkoani Tanga, Ligubi aliyekuwa katika safari
zake vijijini alimkuta mwanaume akitoka shambani akiwa amebeba
radio,lakini mkewe mjamzito alikuwa na mzigo wa kuni kichwani,mgongoni
kambeba mtoto na mikononi kashika majembe mawili.

Amina Mbughuni (44) mkazi wa mtaa wa Bomani Wilayani hapa,alisema Mkuu
huyo wa Wilaya anastahili pongezi za pekee kwa kitendo chake cha
kumuonea huruma mwanamke mwenzetu kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

“Haya mambo yanafanyika sana hasa vijijini,na sisi huku tunaona ni
kitu cha kawaida tu,wanaume wanaona wao ni watu wa kustarehe na sisi
wa kumenyeka na kazi nyingi”alisema Amina.

Alisema mfumo dume umekithiri katika vijiji vya Wilaya ya Handeni na
kwamba wanawake hawana maamuzi hata katika kupanga mambo ya uzazi wa
mpango na ndiyo maana maambukizi ya ukimwi yamekuwa yakishamiri.

Mbuguni ambaye ni mjasiliamali alwaomba viongozi wengine kuiga m fano
wa Ligubi kwani watasaidia kuleta mabadiliko katika suala zima la
unyanyasaji wa kijinsia.

Wanawake hao walisema ili kuleta mabadiliko Serikali inapaswa
kuwasomesha maafisa maendeleo ya jamii wengi na kuwasamabaza vijiji
ili waweze kutoa msaada wa elimu ikiwamo kuwawezesha wanawake kutambua
haki zao za msingi.



Burhani Yakub,Handeni.

WILAYA ya Handeni inakadiriwa kuwa na zaidi ya watoto 6800 yatima
wakiwamo wanaoishi katika mazingira hatarishi pamoja na walea ambao
wazazi wao wamekufa kwa ugonjwa wa ukimwi.

Mratibu wa mpango shirikishi wa kudhibiti ukimwi Wilaya ya
Handeni,Thomas Mzinga, alitoa taarifa hiyo juzi wakati akizungumza na
waandishi wa habari waliokuwa Wilayani hapa kujifunza juu ya
unyanyasaji,unyanyapaa na ukatili wa kijinsia na masuala ya ukimwi
yanayoendeshwa na Chama cha waandishi wa habari za ukimwi (Ajat)

Alisema idadi hiyo ya watoto yatima inatokana na kuendelea kuongezeka
kwao kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele hivyo yamefanyika makadirio
ya sensa iliyofanyika mwaka 2008 chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya
na Mustawi wa jamii ambapo walikuwa 5200.

“Idadi ya watoto yatima Wilayani hapa imekuwa ikiongezeka kila kukicha
licha ya kuwa takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya ukimwi yameanza
kupungua”alisema Mzinga.

Alisema kitaalamu ni kuwa licha ya kwamba maambukizi yameanza kupungua
lakini idadi ya wazazi wanaoendelea kufa ni wale wanaoishi na virusi
vya ukimwi ambavyo waliambukizwa miaka ya nyuma.

Mratibu huyo alisema katika kukabiliana na tatizo la watoto yatima na
wanaoishi katika mazingira magumu,Serikali imejikita katika
kuhakikisha wanapata elimu ambapo imekuwa ikiwalipia ada na
kuwanunulia vifaa vya shule.

Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2009/2010 Halmashauri ya
Wilaya ya Handeni ilipangiwa kupewa kiasi cha sh 57 milioni kwa ajili
ya shuhguli za kupambana na ukimwi ambapo katika robo ya kwanza
ziliwasilishwa sh 32 milioni.

Kwa mujibu wa maelezo ya maratibu huyo ni kuwa sh 32 milioni
zilizowasilishwa zilitumika kwa ajili ya kulipia ada na kuwanunulia
wanafunzi yatima waliopo katika shule mbalimbali za msingi na
sekondari.

MWISHO

No comments: