SAKATA LA MJAMZITO KUJIFUNGULIA KICHAKANI,MUUGUZI ATOWEKA KITUONI,
Na Anthony Mayunga-Serengeti.
SIKU chache tu baada ya sakata la muuguzi wa Zahanati ya Maji moto
kata ya Busawe wilayani hapa Devotha Thomasi kumfukuza mjamzito na
kujifungulia kichakani,ametoweka kwa muda wa siku nne zahanati
haijafunguliwa.
Kitendo hicho kinachoendelea kuwatesa wakazi wa kata hiyo ambao
wanategemea Zahanati hiyo kwa ajili ya huduma ,licha ya kuwepo
matatizo mengi ya kiutendaji.
Mwananchi Jumapili ilielezwa na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho
Johannes Masirori kuwa muuguzi huyo alitoka siku moja tu baada ya tume
iliyoundwa kumchunguza kumaliza mahojiano.
Alisema kuwa toka julai 7 hakuna huduma inayotolewa hapo na hawajui
muuguzi yuko wapi kwa kuwa amekuwa na tabia ya kutoka bila kuagakwa
madai kuwa hawajibiki kwao
“Hapa unadhani nchi haijapata uhuru,maana huduma za afya kama
inavyohubiriwa na viongozi ni tatizo kubwa sana,watu wanafika
kulalamika kwa kukosa huduma,wanalazimika kwenda Iramba zaidi ya
kilometa 30 ,wilaya inajua kilio chetu lakini hawajachukua
hatua,”alisema.
Alibainisha kuwa Zahanati hiyo inategemewa na vijiji vingi ,kufungwa
kwake kunazidi kuwatesa wagonjwa,hasa wanawake wajawazito na watoto
chini ya miaka mitano.
Alisema kuwa kwa kuwa huduma hiyo ni ya msingi sana kwa jamii ,uongozi
wa wilaya unatakiwa kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha wanaachana
na tabia ya kulindana bali uwajibikaji.
“Sijui kwa nini wanalinda kwenye maisha ya watu,hilo lililotokea ni
moja tu likajulikana ,yapo mengi makubwa yanajitokeza hajawekwa
wazi,hivyo uwajibikaji utaaidia kunusuru maisha ya watu,”alisema
Mwenyekiti.
Alipotafutwa na Mwananchi jumapili kwa njia ya simu muuguzi huyo
alikiri kutokuwepo kituoni hapo mpaka jumatatu julai 12.
“Niko Mugumu nimekuja kwa matatizo ,nimefunga kwa sababu niko mwenyewe
sasa nitafanyaje mimi,ni kwa sababu ya matatizo yaliyojitokeza
kazini,”alisema.
Kuhusu matatizo yaliyojitokeza kituo kwake alikiri kuwa tume imeundwa
kumchunguza ,lakini anadai yamebebwa na masuala ya siasa kwa kuwa mme
wake anatarajia kugombea udiwani mwaka huu.
“Ni kweli huyo aliyepata matatizo alikuja kwangu nilimwelekeza aende
kituo cha afya Iramba ,kwa kuwa mimba ilikuwa changa na matatizo
,baadae nikasikia mambo kuwa nimemfukuza,”alisema.
Aliongeza kuwa tatizo hilo lilijitokeza kutokana na kuwa mmoja hapo na
kuwa walimkuta akiwa chumba cha chanjo,na kushindwa kuwahudumia na
kuwaelekeza eneo husika,”mimi nasema siasa inaniumiza maana hili
natengenezewa tu,”alidai.
“Kwa kweli mimi ninapata shida sana,niko pekee yangu nimeomba tuwe
wengi,maana naumwa Bp hupanda kila wakati nashindwa kufanya
kazi,lakini wanasema kuwa mimi nawapiga vita wanaoletwa hapa ili niwe
pekee yangu,”alilalama.
Alikiri baada ya sakata hilo tayari ofisi imempanga muuguzi mwingine
kwenda kituoni hapo na ataripoti julai 12 ,kutoka zahanati ya Maburi.
Kuhusu kutumia muda mwingi kufanya kazi zake za kuuza dawa .alidai
kuwa anaifanya baada ya masaa ya kazi ,”duka ninalo lakini nafanya
baada ya masaa ya kazi,”alisema.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Kimulika Galikunga,Mganga mkuu
Dk Salum Manyatta,na katibu wa afya wa wilaya Peter Shilingi
hawakupokea simu zao licha ya kuita kwa muda mrefu ili kutoa ufafanuzi
huo.
Juni 28 mwaka huu muuguzi huyo anadaiwa kumfukuza Esther Thadeus
aliyefika zahanati hapo kwa ajili ya kujifungua,na kulazimika
kujifungulia kichakani ambapo mtoto alifariki muda mfupi kutokana na
kukosa huduma.
Tukio hilo liliibuliwa na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho na
kutaarifu uongozi wa wilaya waliolazimika kuunda tume ya uchunguzi
,ambayo haijatoa majibu.
Juhudi za kuwasaka zinaendelea ili kupata majibu ya tume na msimamo wa wilaya .
Mwisho.
No comments:
Post a Comment